MAHAKAMA YA MAFISADI – RASIMU YA KANUNI ZINAZOPENDEKEZWA ZA MWENENDO WA KESI KATIKA MAHAKAMA MAALUM YA MAKOSA YA UFISADI NA KIUCHUMI MAARUFU KAMA MAHAKAMA YA MAFISADI

Haya ni baadhi ya mambo muhimu yaliyopo kwenye rasimu ya kanuni za mwenendo wa Mahakama maalum ya makosa ya ufisadi na makosa ya kiuchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi. Kanuni hizi bado hazijapitishwa kuwa sheria, lakini bado ni muhimu kufahamu zinaongelea mambo gani.

Kanuni zinaunda kitengo maalum cha Mahakama Kuu kwa ajili ya makosa ya kiuchumi na ya ufisadi. Masijala kuu itakuwa Dar es salaam na vile vile kutakuwa na masijala ndogo katika sehemu mbalimbali za Tanzania ambazo kwa ujumla zitahudumia karibu mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mashitaka yakifunguliwa yatapelekwa kwanza mahakama ya chini ndani ya siku saba kwa ajili ya hatua za awali ambazo ni pamoja na mshitakiwa kusomewa mashitaka, kusomewa maelezo au nyaraka za ushahidi ambao utatumika dhidi yake, na kuelezwa haki zake kuhusiana na mashitaka hayo. Hatua hii inafahamika kama committal proceedings.

Baada ya hapo mshitakiwa atapelekwa kwenye Mahakama hiyo maalum kwa ajili ya kuendelea na hatua zinazofuata. Kesi inatakiwa imalizike kusikilizwa ndani ya miezi tisa baada ya kumalizika kwa committal proceedings. Hata hivyo, katika mazingira ya kipekee sana Mahakama inaweza kuongeza muda huo lakini si zaidi ya miezi sita.

Katika Mahakama hii si lazima shahidi awepo Mahakamani wakati anatoa ushahidi, bali anaweza kutoa ushahidi wake kwa njia ya mawasiliano ya video. Gharama za njia hiyo zitabebwa na upande ulioomba kutumia njia hiyo ya kutolea ushahidi.

Kanuni pia zinatoa ulinzi kwa mashahidi. Katika mazingira ya kipekee sana, upande wa mashitaka unaweza kuomba ruhusa ya kuficha utambulisho (identity) wa shahidi ambaye anaweza kuwa hatarini, hadi pale ambapo shahidi huyo atapatiwa ulinzi na Mahakama. Maombi hayo yanaweza kufanyika kwa siri (in camera).

Baadhi ya njia za kuficha utambulisho wa shahidi ambazo zinaweza kuruhusiwa ni pamoja na kuondoa taarifa za shahidi huyo kwenye kumbukumbu za Mahakama, kuhakikisha taarifa za shahidi huyo hazitolewi kwa umma, kumpa shahidi huyo majina bandia na kuzuia umma na waandishi wa habari kuwepo wakati shauri likiendelea.

Sambamba na hilo, ushahidi au majina ya watu ambao ushahidi wao umesikilizwa kwa siri hayatachapishwa kwenye gazeti lolote au chombo kingine chochote cha habari. Hata hivyo, taarifa hizo zinaweza kuchapishwa kwenye law reports au majarida ya kitaalamu kwa nia njema kwa ajili ya kusambazwa kwa wanajumuiya ya taaluma ya sheria.

Vilevile, kanuni zimetoa tafsiri pana ya maana ya mshahidi waliopewa ulinzi ambapo tafsiri hiyo itajumuisha ndugu au watu wenye uhusiano na mashahidi hao.