Suala la kupima DNA linazidi kuwa na umuhimu wa pekee miongoni mwa Watanzania kadiri siku zinavyokwenda. Hivyo tumeona tukudokeze machache juu ya sheria inavyosema.

 

Mambo haya ni kwa mujibu wa sheria ya DNA za binadamu ya mwaka 2009 (Human DNA Regulation Act, 2009).

 

Nani anaruhusiwa kuomba vipimo vya DNA kufanyika:

 1. Mahakama, iwapo kuna mgogoro mbele yake.
 2. Wakili.
 3. Afisa ustawi wa jamii.
 4. Afisa maendeleo ya jamii.

Wahusika waliotajwa kwenye namba 2 hadi 4 wanaruhusiwa kuomba vipimo kama DNA hiyo inahusu mambo ya kisheria ambapo hakuna mgogoro.

 1. Polisi mwenye cheo cha inspekta au cheo cha juu yake.
 2. Taasisi za kiutafiti ambazo zimepewa mamlaka ya kufanya tafiti kwenye DNA za binadamu.
 3. Mkuu wa Wilaya, iwapo kuna maafa yametokea.
 4. Mtabibu, kwa madhumuni ya kitabibu tu.

Kabla afisa anayechukua sample ya DNA hajachukua sample hiyo, afisa huyo anatakiwa amweleze mtolewa sample au mwakilishi wake haki zake. Baada ya hapo mtolewa sample au mwakilishi wake ataweka saini fomu maalum kuonesha kuridhia.

Hata hivyo sample za DNA zinazotolewa kutoka kwa wafu, wahalifu au kwa amri ya mahakama hazitahitaji ridhaa ya mtolewa sample au mwakilishi wake.

 

Sample ya DNA inaweza kutolewa kwenye vitu vifuatavyo:

 1. Mate
 2. Nywele yenye mzizi
 3. Haja ndogo
 4. Haja kubwa
 5. Damu
 6. Meno
 7. Ngozi
 8. Mifupa
 9. Shahawa
 10. Maji ya uke
 11. Vitu vinavyoaminika kuwa na masalia ya vyanzo vilivyotajwa hapo juu
 12. Kitu kingine chochote, tishu ya binadamu, au sehemu yoyote ya mwili wa binadamu kama itakavyobidi.

 

Hairuhusiwi kutolewa sample ya DNA ya sehemu za ndani/za siri kama sample ya sehemu ya wazi inapatikana kirahisi.

 

Uchukuaji wa sample za DNA unatakiwa kufanyika kistaarabu na kwa kuheshimu utu.

 

Sample ya DNA inapochukuliwa inabaki kuwa mali ya mtoa sample.

 

Hairuhusiwi kumfanyia mjamzito kipimo cha DNA isipokuwa kwa sababu za kidaktari tu.

 

Hairuhusiwi kuchukua sample ya DNA ya mtoto (mtu mwenye miaka chini ya 18), au mtu mwenye ugonjwa wa akili au mtu ambaye kwa wakati husika akili yake haifanyi kazi vizuri mpaka kuwe na idhini ya kimaandishi kutoka kwa mzazi au mlezi au mwakilishi wake.

 

Kanuni zimeainisha matendo mbalimbali ambayo yakifanywa yatakuwa ni makosa na adhabu yake ni kulipa faini isiyopungua TShs. 5,000,000 au kifungo cha muda usiopungua miaka mitatu na usiozidi miaka mitano. Adhabu pia inaweza kuwa ya kifungo na faini kwa pamoja. Baadhi ya makosa hayo ni:

 1. Kubadilisha sample ya DNA
 2. Kuchukua sample ya DNA bila ruhusa ya maandishi
 3. Kufanya utafiti wa DNA bila kibali
 4. Kukusanya sample za DNA kwa nguvu au kwa kutumia pesa
 5. Kununua sample ya DNA kutoka kwa mtoa sample
 6. Kutuma sample ya DNA nje ya nchi kwa uchunguzi bila kibali

Hayo ni machache tu kuhusu sheria hii na yapo mengine mengi zaidi. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia info@matrix.co.tz