Kesi ya kusingiziwa inaweza kumpatia mtu fidia kubwa ya kifedha, kama TShs. 50,000,000/-
Kumsingizia mtu kesi ya jinai na kumsababishia kuwekwa rumande ni kosa ambalo fidia yake inaweza kufika hadi TShs. 50,000,000/-. Kosa hilo linafahamika kama false imprisonment na liko katika kundi la makosa dhidi ya mtu ambayo yanajulikana kwa ujumla kama Torts. Kosa la false imprisonment maana yake ni kuzuia uhuru wa mtu kwa kumfungia mahali bila uhalali.
Tuangalie kesi ya Augustino Peter Mmasi v. Tausi Selemani iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, mwezi April, 2015. Mnamo tarehe 12/05/2006, majira ya saa kumi na mbili asubuhi, mdogo wake Augustino aitwaye Paul Mmasi alikutwa mferejini akiwa amekufa. Kesho yake majira ya saa nane usiku Tausi alifuatwa nyumbani kwake na polisi watatu waliokwenda kwa taxi, na wakiwa wameambatana na kakake Austino aitwaye Sylvanus.
Polisi walipowasili nyumbani kwa Tausi walimkamata na kumtuhumu kwa mauaji ya Paul, ila hawakumpa maelezo zaidi ya tuhuma hizo. Polisi hao wakamweka Tausi ndani ya ile taxi na kumpeleka moja kwa moja nyumbani kwa Augustino. Walipofika, polisi mmoja akamwita Augustino na kumuuliza kama Tausi ndiye muuaji, Augustino akawajibu kwamba ndiye huyo na waondoke nae.
Tausi akapelekwa kituo cha polisi cha Buguruni ambapo aliwekwa rumande. Baada ya kukaa humo kwa siku tano ndipo akaelezwa vizuri sababu za kukamatwa kwake. Alitoa maelezo yake na kueleza kwamba hahusiki na mauaji hayo. Baada ya kutoa maelezo, Tausi hakupelekwa mahakamani, bali aliendelea kuwekwa rumande kwa siku kadhaa na baadaye polisi wakamwachia na kumweleza kwamba hana hatia. Kwa ujumla alikaa rumande kwa siku 38.
Baada ya kuachiwa, Tausi alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania akimdai Augustino fidia ya TShs. 500,000,000/- kwa kosa la false imprisonment, yaani kumsababishhia kuwekwa rumande bila uhalali wowote. Augustino alikana kabisa kuhusika na kukamatwa kwa Tausi. Alidai kwamba baada ya kupata taaria za kifo cha mdogo wake, alienda eneo la tukio, akautoa mwili wa mdogo wake kutoka kwenye mfereji na kuuweka pembeni ya barabara, kisha akarudi nyumbani kuandaa mazishi. Alikana kabisa kuwataarifu polisi chochote.
Mahakama Kuu iliona kwamba ushahidi wa Tausi ulikuwa una nguvu, wakati ushahidi wa Augustino haukuwa na nguvu kutokanana kwamba maelezo yake yalikuwa hayajitoshelezi. Hivyo Mahakama ikaamua kwamba Augustino ndiyo ambaye alisababisha kukamatwa kwa Tausi na hivyo kumwamuru Augustino amlipe Tausi fidia ya TShs. 50,000,000/-. Augustino hakuridhika hivyo akakata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa akisisitiza kwamba hana hatia.
Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba kweli Augustino ndiye aliyesababisha Tausi kukamatwa. Mahakama ilienda mbele zaidi kwa kueleza nani ana jukumu la kuleta ushahidi wa kuthibitisha kosa la false imprisonment, na hapa ndipo palipomwangusha Augustino.
Mahakama ilifafanua kwamba kazi ya Tausi ni kuthibitisha kwamba aliwekwa kizuizini, basi, na Tausi alikuwa ametekeleza kazi hiyo. Baada ya hapo, jukumu lilihamia kwa Augustino kuthibitisha kwamba kulikuwa na uhalali wa kumsababishia Tausi kizuizini. Hii kwa kiingereza inaitwa burden of proof.
Makakama ilihitimisha kwamba Augustino hakuwa amefanya chochote cha kuthibitisha kwamba ilikuwa ni halali kumsababisha Tausi kuwekwa kizuizini. Kutokana na hivyo, Mahakama ikakubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba Augustino ana hatia na hivyo amlipe Tausi fidia ya TShs. 50,000,000/- kama ilivyokuwa imeamuliwa toka mwanzo na Mahakama Kuu.
Uamuzi huu ni fundisho kwa watu wenye tabia ya kusingizia watu wengine kesi za jinai kwa ajili ya kuwakomoa.
Kama una maswali au maoni yoyote tuandikie kupitia [email protected]